ABIRIA 10 waliokuwa wamepanda meli ya FB Matara wamenusurika kifo baada ya meli hiyo kukumbwa na dhoruba kali katika visiwa vya Lukoli na Kerebe na kuzama.
Meli hiyo inayomilikiwa na Kampuni ya Mkombozi Fishing and Marine Transport Ltd, ilikuwa imebeba tani 280 za sukari kutoka Kiwanda cha Sukari Kagera kichopo Bukoba kwenda jijini Mwanza. Tani hizo za sukari ni sawa na magunia 5,600 yenye kilo 50 kila moja.
Kwa mujibu wa watu walionusurika ambao ni wafanyakazi wa meli hiyo, meli hiyo ilizama jana saa 10:30 alfajiri na kwamba chanzo cha ajali hiyo ni dhoruba kali.
Mmiliki wa meli hiyo aliyetambuliwa kwa jina moja la Gitana, amethibitisha kuzama kwa meli hiyo na kueleza kuwa wafanyakazi wake 10 wamenusurika.
Alisema mzigo uliozama ulikuwa ni wa mfanyabiashara wa jijini Mwanza aliyemtaja kwa jina la V. H. Shah.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, George Mayunga, amelithibitishia Tanzania Daima kuzama kwa meli hiyo, na kwamba wanaendelea kufuatilia.
Katika tukio jingine, watu watano wamenusurika kufa baada ya boti ya uvuvi waliyokuwa wamepanda kuzama katika ukanda wa bahari ya Hindi.
Kwa mujibu wa shuhuda wa ajali hiyo, Selemani Tandani ajali hiyo ilitokea katika eneo la Mafia, wakati wavuvi hao walipokuwa wakitoka katika kisiwa cha Nyororo kurejea Dar es Salaam.
Tandani aliiambia Tanzania Daima kwa njia ya simu kuwa tukio hilo lilitokea kwenye kisiwa hicho wakati boti hiyo ikiwa na samaki waliovuliwa, wanaokadiriwa kuwa na thanani ya sh milioni 9.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, hakupatikana kuthibitisha tukio hilo.
#SHARE THIS NEWS AND WIN!!!#
0 comments