,

WANAUME KUBALINI TU KUCHUNWA, NI KAWAIDA...

10:31 PM

NI wiki nyingine tofauti kabisa na wiki iliyopita ambapo tunakutana tena kupitia safu hii nikiamini kwamba umzima na unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku kama kawaida.
Mpenzi msomaji, wapenzi wako wa aina tofauti. Kuna wale ambao mwanamke anafanya kazi mwanaume hana kazi, mwanaume ana kazi na mwanamke hana kazi ama wote wanafanya kazi.
Katika mazingira hayo, fahamu kwamba mpenzi wako ana haki ya kukuchuna kimtindo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha shida ndogondogo hazimtesi.
Hutakiwi kuwa mbahili hata kidogo na unachotakiwa kufanya ni kumpatiliza katika mahitaji yake muhimu pale atakapohitaji.
Hapa sizungumzii kwamba mwanaume ndiye anayetakiwa kumfanyia hayo mpenzi wake bali hata mwanamke pia anatakiwa kumfanyia mambo fulani mpenzi wake kwa kutumia kipato chake.
Kuna baadhi ya wanawake wao siku zote ni watu wa kuwachuna tu wapenzi wao licha ya kwamba wao pia wana vipato vyao. Si wanawake tu bali pia kuna hata wanaume ambao ubahili wao umezidi kipimo kiasi kwamba hawezi kuwapa wapenzi wao nafasi za kuwachuna. Unamkuta mwanaume anafanya kazi na anapata mshahara mnono tu lakini mpenzi wake akimgusia tu kuwa ana shida na kiasi f’lani cha pesa, anakuwa mgumu.
Ni kweli mapenzi na pesa ni vitu viwili tofauti lakini mpenzi wako akikulilia shida kama unao uwezo msaidie. Hivi unadhani kama usipomsaidia wewe nani amsaidie? Au unataka atafute mwanaume mwingine wa kumchuna?
Ninachoona hapa ni baadhi ya wanaume kuhisi kwamba kuwasaidia wapenzi wao pale wanapolia shida ni sawa na kukubali kugeuzwa mabuzi wa kuchunwa.
Nadhani ifike wakati tukubali wapenzi wetu nao watuchune wakiwa na sababu za msingi za kufanya hivyo. Tuwe na mioyo ya kuwasaidia na wakati mwingine usisubiri mpaka mpenzi wako awe na shida. Ukiona katika fedha zako kuna ziada, waweza kuamua siku moja ukamnunulia zawadi yoyote ambayo unaona inafaa, mkaenda ‘out’ mkatumia, hayo ndiyo mapenzi.
Lakini katika hili naomba nitahadharishe kitu. Unaweza kuwa na mpenzi ambaye anakupa uhuru wa ‘kumchuna’, kila wikiendi anakutoa ‘out’, anakupatiliza katika kile unachotaka lakini akawa hana mapenzi ya dhati.
Naomba niseme tu kwamba, kwenye suala la matumizi ya fedha zetu, achilia mbali wale walio katika uhusiano wa kawaida, hata wale waliooana wanaweza kusaidiana katika kuchangia matumizi ya ndani ya familia kutokana na kila mtu kuwa na kipato.
Maisha ya sasa ni kusaidiana na si kutegemeana, labda ziwepo sababu za msingi za mume kutegemea kipato cha mke ama mke kutegemea kipato cha mume.
Lakini tuna kila sababu ya kukaa chini na kujiuliza, kwa nini baadhi ya watu wanakuwa wabahili kupindukia kwa wapenzi wao?
Kweli mpenzi wako anakutembelea kisha unashindwa hata kumnunulia maji ya baridi achilia mbali soda? Anaondoka unashindwa hata kumuambia chukua basi 1000/= uongezee nauli.
Sawa! Tunajua kwamba kuna ulazima wa kuwa makini katika kila shilingi unayoipata, lakini umakini huo usizidi kipimo mpaka ufikie hatua hiyo.
Nasema hivyo kwa sababu, kila utakachokuwa unamfanyia mpenzi wako kinadhihirisha mapenzi ya dhati uliyonayo kwake, pia unaonesha kumjali.
Sisemi kwamba ni lazima umpe mpenzi wako pesa ama kitu f’lani kuonesha kwamba unampenda lakini kufanya hivyo kunaongeza chachu ya penzi lenu.
Hilo ni kwa wale wenye uwezo kidogo kifedha ila kwa wale wenzangu na mimi wasio na uwezo, hawatakiwi kujali wala kujiona kwamba labda kutowapa wapenzi wao fedha ama kuwanunulia zawadi wataonekana kwamba hawawapendi. Kumbuka mapenzi ya dhati ni yale yanayotoka moyoni.
Katika hili pia niwatahadharishe tu kwamba, unapomuona mwanaume ama mwanamke ni mwepesi sana wa kukupa pesa hata pale ambapo huzihitaji, penzi lake kwako litakuwa na walakini. Yawezekana anataka kununua penzi kutoka kwako wakati hata siku moja penzi halinunuliwi.
Ila mpenzi wako anapokuwa na uwezo kifedha, kisha akawa mgumu sana kukusaidia pale unapokuwa na matatizo huyo hakupendi na kama anakupenda basi atahakikisha kwamba na wewe unakifaidi kipato chake.
Kwa kuhitimisha niseme tu kwamba, mapenzi ni baina ya wewe na mpenzi wako. Mapenzi ni kusaidiana, mapenzi pia ni kupeana raha. Mnapojaaliwa kuwa na uwezo kidogo, zitumieni fedha zenu katika kufanya mambo yatakayoyaboresha maisha yenu.
Msaidie mpenzi wako na kamwe usioneshe ubahili kwake kwani kufanya hivyo ni wazi kwamba ataona kama unamyeyusha na hakawii kupunguza mapenzi yake kwako.

GPL
#SHARE THIS NEWS AND WIN!!!#

You Might Also Like

0 comments

JIUNGE UPATE HABARI

Jisajili Sasa upate E-mail ya Kila Tunachochapisha....