,

PICHA!! KIKWETE ALIPOTEMBELEA KIWANDA CHA TAJIRI NO.1 AFRICA CHA DANGOTE NIGERIA

12:20 AM



 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametumia siku nzima ya  Ijumaa, Mei 9, 2014, kutembelea kiwanda kikubwa zaidi cha saruji kuliko kingine chochote duniani cha Dangote Cement Obajana Plant na kinachomilikiwa na tajiri mkubwa zaidi wa Afrika, Bwana Aliko Dangote, ambaye pia anajenga kiwanda kikubwa cha saruji mjini Mtwara.
 
Akiandamana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Abdallah Kigoda, kwa siku nzima, Rais Kikwete ametembelea kiwanda hicho cha Saruji cha Dangote kilichoko katika eneo la Obajana, Jimbo la Kogi, kilomita 400 kaskazini mashariki mwa mji maarufu wa kibiashara wa Nigeria, Lagos. 
 
Rais Kikwete ambaye alikuwa nchini Nigeria kuhudhuria Kongamano ya Uchumi Duniani-Afrika (WEFA) mwaka huu aliamua kutumia siku yake ya mwisho ya ziara yake ya siku tatu nchini humo, kwa kutembelea uwekezaji mkubwa wa mwekezaji ambaye ameanza ujenzi wa kiwanda cha saruji cha Mtwara ambacho kitakuwa kiwanda kikubwa zaidi cha saruji kuliko kingine chochote katika Tanzania, kikiwa na uwezo wa kuzalisha tani za kimetriki milioni tatu kwa mwaka. 
 Rais Kikwete ambaye alipokewa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kiwanda hicho na Bwana Dangote mwenyewe, na kuanza ziara yake kwa kutembelea machimbo ya kiwanda hicho ambayo yako kilomita tisa kutoka kiwandani ambako malighafi ya kiwanda hicho husafirishwa kwa madaraja na mikada maalum hadi kiwandani. 
Bwana Dangote amemwambia Rais Kikwete kuwa kwa sasa Kiwanda cha Obajana kinazalisha tani za kimetriki milioni 10.25 kwa sasa kwa mwaka na hivyo kukifanya kiwanda hicho kuwa kiwanda kikubwa zaidi cha saruji duniani kilichoko katika eneo moja na kuwa baada ya upanuzi unaoendelea kufanywa kwenye kiwanda hicho, uwezo wake wa uzalishaji utaongezeka na kufikia tani za kimetriki 13.0 kwa mwaka ifikapo mwakani 2015. 
Bwana Dangote amemwambia Rais Kikwete kuwa kiwanda hicho kilicho kwenye eneo la kilomita za mraba saba kitakuwa kimegharimu kiasi cha dola za Marekani bilioni 2.5 wakati upanuzi wake utakapokamilika. 
Kwa sasa kiwanda hicho kina biashara ya dola za Marekani bilioni mbili kwa mwaka. Bwana Dangote amemwambia Rais Kikwete kuwa kiwanda hicho kilichoanza kujengwa mwaka 2003 na kukamilishwa mwaka 2006 na hatimaye kuzinduliwa na Rais Olusegun Obasanjo Mei 12, mwaka 2007, wiki mbili kabla ya kustaafu Urais wa Nigeria, kinaajiri watu 800 kwa wakati mmoja na hivyo kuwa miongoni mwa waajiri wakubwa zaidi katika Nigeria. 
 
“Mheshimiwa Rais, ili kuelewa vizuri mchango wa kiuchumi na kijamii za kiwanda hiki na viwanda vyetu vingine katika maeneo mengine ya Nigeria, unahitaji kukumbuka kuwa kabla ya kuanza kujenga kiwanda hiki, Nigeria nzima ilikuwa na uwezo za kuwazalisha tani za kimetriki za saruji milioni1.5 tu, wakati huo chini ya miaka 10 iliyopita. 
 
"Tunataka kufikia hatua ya kuhakikisha kuwa eneo la Afrika Magharibi na hata Bara letu la Afrika linaacha kabisa kuagiza saruji nje ya Bara letu. Na tutafikia huko.” 
 
Mbali na Kiwanda cha Obajana, Kampuni ya Saruji ya Dangote inazalisha saruji katika maeneo mengine mawili ya Nigeria ambalo uzalishaji wa jumla wa maeneo hayo matatu ni tani za metriki 20.25 kwa mwaka. Amesema Bwana Dangote kuwa ili kuweza kuwa na uhakika wa umeme, uongozi wa kiwanda hicho uliamua kuzalisha umeme wake kwa ajili ya kiwanda hicho kwa kujenga, miongoni mwa hatua nyingine, bomba ya kilomita 92 la kusafirisha gesi kutoka Ajaokuta hadi kwenye kiwanda hicho. 
 
Alipoulizwa na Rais Kikwete kama wanategemea kwa namna yoyote umeme wa taifa, Bwana Dangote alijibu kwa furaha, “hatujaunganishwa kwenye gridi ya taifa na tunadhani hili ni jambo zuri kwa sababu hatua tulizochukua zinatuhakikishia umeme wakati wote na kwa kiwango ambacho tunakihitaji. Tunatumia gesi ama diseli yetu wenyewe. Na wala siyo umeme tu, hata miundombinu ya eneo hilo kiliwemo daraja hili kubwa linalonganisha eneo la machimbi na kiwanda, tumejenga sisi Mheshimiwa Rais.” 
 
 Bwana Dangote amesema kuwa mbali na kujenga miundombinu ya umeme wake, kiwanda hicho pia kimejenga bwawa lake lenyewe kwa ajili ya huduma ya maji kusaidia uzalishaji wa saruji bila kutegemea huduma ya maji ya Serikali. 
 
Aidha, bwawa hilo linatoa huduma ya maji kwa jamii inayozunguka kiwanda hicho. Mbali na shughuli za kiwanda, Kampuni ya Bwana Dangote inashiriki kwa karibu sana shughuli za jamii inayozunguka kiwanda ambacho kwa sasa imeanzishwa miji midogo saba katika eneo lililokuwa pori lenye nyumba 50 za wenyeji tu kabla ya shughuli za kiwanda hicho kuanzishwa. 
 
Bwana Dangote amemwambia Rais Kikwete kuwa kampuni yake inatoa shughuli za elimu, maji na umeme kwa wananchi ambao wanazunguka kiwanda ambacho tokea kuanzishwa kwake limevutia mabenki 13 ambayo yameanzishwa matawi yake katika eneo la kiwanda. 
 
“Mheshimiwa Rais, mbali na nyumba za wafanyakazi, tunawajengea hata nyumba za kuishi wananchi wanaozunguka eneo hili ambao wanatuunga mkono sana.” Mbali na kutoa huduma nyingine za kijamii, Kampuni ya Saruji ya Dangote inajenga taasisi kubwa ya elimu ya Dangote Academy ambayo itatoa elimu na mafunzo ya kiufundi kwa ajili ya kuandaa wafanyakazi wa kiwanda hicho na watoto wa jamii inayozunguka kiwanda hicho.
 
 Ili kuhakikisha kuwa upanuzi wa kiwanda hicho unakwenda kwa kasi kubwa zaidi, Bwana Dangote ameagiza kiasi cha malori 6,000 kutoka China kusaidia ujenzi na pia amechukua uamuzi usiokuwa wa kawaida wa kuagiza maelfu ya vibarua kutoka nchi hiyo hiyo ya China kushiriki katika ujenzi huo na kuumaliza kwa haraka. 
 
Bwana Dangote amemwambia Rais Kikwete kuwa kampuni yake inafanya jitihada kubwa kuhakikisha kuwa Rais Kikwete anakifungua kiwanda cha saruji cha Mtwara kabla ya kustaafu mwishoni mwa mwaka ujao. 
 
Mbali na Nigeria na Tanzania, Bwana Dangote ana viwanda ama anajenga viwanda vya saruji ama na shughuli za saruji katika nchi 14 za Afrika ikiwamo Ethiopia, Zambia, Mozambique, Kenya, Senegal na Sierra Leone, Afrika Kusini, Congo (Brazzaville), Cameroun, Ghana, Liberia na Ivory Coast.
  Mbali na shughuli za uzalishaji wa saruji, Bwana Dangote ambaye anakubaliwa kuwa tajiri mkubwa zaidi katika Afrika kwa thamani ya dola za Marekani bilioni 25 yeye na kampuni yake ya Dangote Group pia ina shughuli za uzalishaji wa sukari, uzalishaji wa chumvi, utengenezaji wa magunia, uzalishaji maji, uzalishaji wa vyakula vya aina mbali mbali, uzalishaji wa mafuta ya kupikia, utengenezaji wa nyanya. 
 
Kwa sasa anaendelea na ujenzi wa kiwanda cha mbolea na kile cha kuzalisha bidhaa za petrol na kemikali. Kampuni ya Saruji ya Dangote – Dangote Cement- ndiyo kampuni kubwa kuliko zote katika Afrika Magharibi kwa sasa ikiwa na thamani ya dola za Marekani bilioni 22.7 kwa tathmini ya mwaka huu baada ya kuongeza thamani yake kutoka dola za Matrekani bilioni14.5 za mwaka jana. Mwishoni mwa ziara hiyo yenye mafanikio makubwa, Rais Kikwete aliondoka Obajana kurejea nyumbani kupitia Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Luanda, Angola ambako jana Jumamosi  alikutana na marais wa nchi hizo kabla ya kurejea nyumbani.
Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akilakiwa na mfanyabiashara na mwekezaji maarufu wa Nigeria Alhaj Aliko Dangote katika uwanja wa ndege wa kiwanda chake cha saruji cha Dangote Cement Obajan Plant kilichoko kilomita 400 Kaskazini Mashariki mwa Lagos alipotembela Mei 9, 2014. Kushoto ni Balozi wa Nigeria nchini Tanzania Mhe. Dkt. Ishaya Samaila Majanbu
Rais Dkt Jakaya Mrisho kikwete akipata maelezo toka kwa mfanyabiashara na mwekezaji maarufu wa Nigeria Alhaj Aliko Dangote wakati akizungushwa kuangalia kiwanda cha saruji cha Dangote Cement Obajan Plant kilichoko kilomita 400 Kaskazini Mashariki mwa Lagos alipotembela Mei  9, 2014.
Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akitembezwa kwenye machimbo ya kiwanda cha saruji cha Dangote Cement Obajan Plant kilichoko kilomita 400 Kaskazini Mashariki mwa Lagos alipotembela Mei 9, 2014. Kwa picha zaidi BOFYA HAPA.


USIACHE KUSOMA HAPA, KARIBU TENA NA TENA. ASANTENI

You Might Also Like

0 comments

JIUNGE UPATE HABARI

Jisajili Sasa upate E-mail ya Kila Tunachochapisha....