ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Full Gospel & Bible Fellowship (FGBF)
lenye makao makuu yake jijini Dar es Salaam, Zakaria Kakobe ameibuka na
kuweka wazi kuwa kuonekana kwa Mwezi Mwekundu (Blood Moon), Aprili 15,
mwaka huu ni ishara kuu ya mwisho wa dunia kama maandiko yanavyosema
katika Matendo 2:17-21, Uwazi linakumegea kwa kina.
Askofu
Kakobe aliyasema hayo juzi kufuatia tukio hilo lililojiri siku tano
kabla ya Sikukuu ya Pasaka ambapo mwezi wote ulipatwa (lunar eclipse) na
kuwa mwekundu kama damu, tukio ambalo pia litatokea tena
mwakani.Kufuatia tukio hilo lenye kuogofya, baadhi ya mitandao ya
kijamii duniani kote imekumbushia maneno ya manabii mbalimbali lakini
zaidi kutoka kwenye Biblia wakisema mwisho wa dunia sasa ni dhahiri.
MSIKIE KWA UNDANI
“Kinachotakiwa kwa watu sasa
ni kuacha maovu na kumrudia Mungu. Ni wajibu wa kila mtu kujiweka tayari
kwa kuokoka kwani bila kufanya hivyo watakaokutwa katika dhambi
watatupwa jehanamu,” alitahadharisha Askofu Kakobe.
Aliongeza kuwa, dalili zote za mwisho wa dunia zilizotajwa katika
Biblia ziko wazi kwa sasa, kama vile hilo la mwezi wa damu, kuzuka kwa
manabii wa uongo, vita ya nchi na nchi na ukoo kwa ukoo lakini akasema
hajui ni kwa nini watu hawataki kuokoka.
NAYE MAMA RWAKATARE
Naye Mchugaji wa Kanisa la
Assemblies of God ‘Mikocheni B’ la jijini Dar, Mama Getrude Rwakatare
alikiri kulijua hilo la mwezi kuwa wa damu na kusema katiba Biblia,
Luka 21:25 Mungu amefafanua kuwa kuna dalili mbalimbali zitajitokeza
siku za mwisho wa dunia na sasa zinaanza kuonekana, akawataka watu
kuomba bila kuchoka.
“Dalili nyingine ni mataifa kupigana, upendo wa wengi kupoa, manabii
wa uongo kuibuka na kadhalika. Haya tunayaona sasa, hivyo watu wote
tumrudie Mungu,” alisema Mama Rwakatare.
NABII SUGUYE PIA
Uwazi lilibahatika kuzungumza
na Nabii Nicolaus Suguye wa Kanisa la Huduma na Neno la Upatanisho
ambaye alisema dalili za mwisho wa dunia ni nyingi ambazo ni mataifa
kupigana, kukosa uhusiano mzuri na kuzuka kwa manabii wa uongo.
NABII GEODAVIE AJUAVYO YEYE
Uwazi lilikwenda
mbele zaidi kwa kuzungumza na kiongozi wa Kanisa la Ngurumo za Upako
lenye makao makuu jijini Arusha, George David ‘GeoDavie’ ambapo alikuwa
na haya ya kusema:
“Suala la kupatwa kwa mwezi na kuwa damu ni ishara ya mwisho wa
dunia lakini nasisitiza kuwa pia ni jambo la kisayansi zaidi.”
Alizidi kusema kuwa kilichoandikwa kwenye Biblia, Luka 21:25 (Tena
kutakuwa na ishara katika jua na mwezi na nyota na katika nchi, dhiki ya
mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake) lazima
kikubalike na kila anayemwamini Mungu.
IMANI MWAKYOMA WA TAG
Mchungaji Imani Mwakyoma
wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Magomeni jijini Dar, yeye
alisema kupatwa kwa mwezi na kuonekana wa rangi ya damu ni mafundisho
ambayo watumishi wa Mungu wamekuwa wakiihubiri kila kukicha.
“Tumekuwa tukihubiri kwa muda wa miaka kumi sasa kwamba mwisho
utafika pale tu ishara ya anga itakapoanza kuonekana, mwezi kuwa wa damu
na jua kuwa giza, siku hizi kila mara jua linapatwa na kuwa giza, bado
nini sasa hapo? Watu wamrejee Mungu,” alisema Mchungaji Mwakyoma.
ASKOFU MALASUSA, KARDINALI PENGO
Baadhi ya
waumini wa kanisa la Romani Katoliki linaloongozwa na Mwadhama Polycarp
Kardinali Pengo na Kanisa la KKT linaloongozwa na Askofu Dr. Alex Gerhaz
Malasusa, walisema watumishi hao wa Mungu mara kwa mara wamekuwa
wakihubiri watu kutubu kwa kuwa siku za mwisho wa dunia zipo dhahiri kwa
sasa.
MCHUNGAJI WA MAREKANI
Naye John
Hagee, Mchungaji wa Kanisa la Cornerstone, San Antonio, Texas Marekani
na mwanzilishi wa muunganiko wa Wakristo nchini Israeli alishawahi kutoa
kitabu akiongozwa na taasisi ya uchunguzi wa anga za juu ya nchi hiyo,
NASA kwa kufanya makadirio kupitia historia ambapo aliandika uhusiano wa
moja kwa moja kati ya kupatwa kwa mwezi na kuwa mwekundu na utabiri wa
Waisrael na wanadamu wote.
NI KARIBU NA PASAKA TU?
Katika kitabu hicho,
Mchungaji Hagee aliandika kwamba, zaidi ya miaka 500 iliyopita kupatwa
kwa mwezi wa damu kulitokea siku ya kwanza ya Sikukuu ya Pasaka mara
tatu tofauti.'
Hata Aprili mwaka huu, mwezi huo ulipatwa na kuwa mwekundu kuelekea
Sikukuu ya Pasaka na itatokea tena mwakani kipindi cha Pasaka.
LAZIMA WATU WAJUE ISHARA
Mchungaji Hagee
alifafanua kwamba kupatwa kwa mwezi ni lazima watu, hasa Wakristo
waelewe ishara hizo. Alisema katika Biblia, Joel: 2 na Matendo ya
Mitume: 2 vyote vimeandika tukio hilo kwamba ndiyo mapito ya dunia
kuelekea mwisho wake.
BAADA YA MATUKIO HAYA
Kwa mujibu wa Markell,
mchambuzi wa mambo ya sayansi, kupatwa kwa mwezi na kuwa wa damu
kutatokea tena katika mpangilio wa Oktoba 8, 2014, Aprili 4, 2015 na
Septemba 28, 2015!
IMANI YA KIKRISTO
Hata hivyo, Markell anasema
kuwa Wakristo wengi wanaamini maneno ya kale kwamba kupatwa kwa mwezi ni
dalili ya ujio wa pili wa Kristo na hivyo kusababisha hofu miongoni mwa
wale ambao hawajui maana halisi japo maelezo ya kisayansi yanafafanua
jambo hili.
Alisema kimsingi, rangi ya mwezi ni nyekundu ambayo ipo katika anga
ya dunia na kama dunia haina anga, moja kwa moja mwezi utafunikwa na
giza.
Markell ambaye anaamini kwamba shetani yupo nyuma ya harakati za
maendeleo, anasema hakuna mtu anayejua ishara za mwezi lakini
alipendekeza kuwa dunia inapaswa kubashiri kwa habari mbaya.
Stori: Andrew Carlos, Haruni Sanchawa na Makongoro Oging’.
#SHARE THIS NEWS AND WIN!!!#
0 comments